Mafunzo Sahihi Ya Uislam

Tuandikie

Yampasa muislam ajiandae kufikiwa na mauti kwa kukithirisha (kufanya sana) matendo mema na kujiepusha na makatazo (vilivyoharamishwa). Vilevile mauti yawe akilini mwake, kwa maneno ya Mtume ((Zidisheni kukumbuka kiondoshacho ladha (yaani mauti))). Hadithi hii imepokewa na Imam Tirmidhi na akaithibitisha usahihi wake Imam Albani katika kitabu chake IRWAA uk. 682.

Anapofariki muislam yampasa yule au wale waliopo pale karibu na maiti kumfanyia mambo yafuatayo:

1. Kuyafumba macho ya maiti huyo kwani Mtume صلي الله عليه وآله وسلم aliyafumba macho ya Abu Salamah alipofariki kisha akasema,((Hakika macho yanafuata roho inapotolewa)). Imesimuliwa na Imam Muslim.

2. Avilainishe viungo vya maiti ili visikakamae.

3. Aifunike maiti hiyo kwa nguo ambayo itasitiri mwili mzima kwa kauli ya Bi ‘Aishah, (Hakika alipofariki Mtume صلي الله عليه وآله وسلم alifunikwa kwa nguo iliyomsitiri kote). Imesimuliwa na Imam Al Bukhariy na Imam Muslim.

4. Waharakishe kuiandaa maiti, kuiosha, kuikafini, kuiswalia na kuizika. Kwani Mtume صلي الله عليه وآله وسلم amesema,((Liharakisheni jeneza)). Imesimuliwa na Imam Al Bukhariy na Imam Muslim.

5. Waizike katika mji au eneo alilofia kwa vile katika vita vya UHUD Mtume صلي الله عليه وآله وسلم (aliamrisha mashahidi wa vita wazikwe pahala pale walipofia wala wasihamishwe). Imepokewa na AHLUS SUNAN (MaImam Abu Dawud, An Nasaaiy, At Tirmidhiy, Ibnu Maajah) na ameithibitisha usahihi wa hadithi hiyo Imam Albani katika kitabu chake cha AHKAMUL JANAIZ uk. 14.

 

[Utangulizi] [Kumuosha maiti] [Kumkafini maiti] [Swala ya jenaza] [Kubeba jenaza na kuzika] [Kuomboleza na taazia]