Swala ya jenaza

Tuandikie

• Swala ya jeneza (maiti) ni FARDHU KIFAAYAH (wanapofanya baadhi ya waislam basi inatosha na si lazima waislam wengine waliobaki kuifanya).

• Inasuniwa kwa Imam wakati wa kumswalia maiti asimame kuelekea kichwani mwake akiwa maiti ni mwanaume (tazama picha na.15).

[Imamu akiwa anaswali huku amesimama akielekea upande wa kichwa cha maiti wa kiume]

PICHA NAMBA 15

 

na kama maiti ni mwanamke basi asimame kuelekea katikati yake (tazama picha na.16).

[Imamu akiwa anaswali huku amesimama akielekea katikati ya maiti wa kike]

PICHA NAMBA 16

 

Hivyo ndivyo alivyofanya Mtume صلي الله عليه وآله وسلم, amesimulia hadithi hii Imam Abu Dawud na ameithibitisha usahihi wake Imam Albani katika kitabu chake cha AHKAMUL JANAIZ.

• Ni sunna Imam kuwa mbele ya maamuma, lakini endapo itakosekana nafasi basi maamuma wasimame kuliani na kushotoni kwake naye awe katikati yao.

• Atakapoanza kuswalisha imam atasema Audhubillah Mina Shaytwaan Rajiim. Kisha atapiga Takbira nne atanyanyua mikono katika takbir ya kwanza. Kisha si lazima kunyanyua mikono katika takbir tatu zilizobaki kwani maswahaba walifanya hivyo. Na si vibaya kwa mtu kunyanyua vile vile.

• Baada ya takbira ya kwanza atasoma Suratul Faatiha na baada ya takbira ya pili atamswalia Mtume kama anavyofanya katika TASHAHUD yaani atasema ((Allahumma swali ‘alaa Muhammad wa’ala aali Muhammad kamaa swalayta ‘alaa Ibraahiym wa’alaa aali Ibrahiyma, Innaka hamiydunmajiyd. Wabaariki a’laa Muhammad….)) Na endapo atafupisha na kusema ((Allahumma swali a’laa Muhammad)) basi pia inafaa Wallahu A’alam.

• Kisha baada ya takbira ya tatu anatakiwa amuombee maiti kwa dua zilizothibiti kutoka kwa Mtume صلي الله عليه وآله وسلم Miongoni mwa dua hizo ni hii ((Allahummaghfir lahu warhamhu, wa'afihi wa’afanhu, wanaqihi minal khatwaayaa kamaa yunaqa athawbul abyadh minnad danas, waabdilhu daaran khayran min daarihi, wa ahlan khayran min ahlihi, wazawjan khayran min zawjihi, waadkhilhul jannah, waa’idh-hu min ‘adhaabil qabri, wamin ‘adhabi nnaar)). Imesimuliwa na Imam Muslim.

• Ama kuhusiana na ASSIQT nacho ni kile kiumbe kilichozidi miezi minne,katika swala kinaombewa msamaha na rehema kwa baba yake kwa kauli ya Mtume صلي الله عليه وآله وسلم, ((ASSIQT kinaswaliwa na kuombewa msamaha na rehema mzazi wake)). Imesimuliwa na Imamu Abuu Dauud na imethibitishwa usahihi wake na Imamu Albani.

• Na kisha baada ya takbira ya nne atanyamaza kidogo na kisha atatoa salamu mara moja tu upande wa kulia kama alivyofanya Mtume S.AW. Imesimuliwa na Imam Al Haakim na kuthibitishwa usahihi wake na imam Albani na pia mtu anaweza kutoa salam upande wa kushoto. Tazama kitabu cha AHKAAMUL JANAIZ cha Imam Albani.

• Atakayepitwa na baadhi ya takbira basi anatakiwa amfuate imam, mathalan amemkuta imam yuko katika takbira ya tatu basi afanye kila kinachofanywa katika takbira hiyo, nayo ni kusoma dua ya kumuombea maiti kisha baada ya takbira ya nne yeye hatatoa salam bali atapiga takbira na kusoma surat fatiha, na halafu atapiga takbira nyingine na kumswalia Mtume صلي الله عليه وآله وسلم na baada ya hapo ndipo atatoa salaam. Hayo yote atayafanya endapo kutakuwa na nafasi, ila akiona jeneza linanyanyuliwa basi ataacha na haidhuru.

• Atakayepitwa au kuchelewa kumswalia maiti, basi atamswalia kaburini, wakati anaiswalia maiti kaburini anatakiwa aelekee kibla na kaburi liwe katikati yake na kibla, ataiswalia kama inavyosikiliwa maiti (tazama picha na.17) kama alivyofanya Mtume صلي الله عليه وآله وسلم Muttafaqun ‘Alayh

[Mtu anaonekana akimswalia maiti kaburini kaburi likiwa mbele yake na huku ameelekea kibla]

PICHA NAMBA 17

 

• Inapendeza vile viele swala ya ghaib, yaani kwa mtu aliyefariki mji au nchi nyingine ikiwa huko aliko hakuswaliwa.

• Waislamu wanaweza kumswalia mtu aliyejiua , jambazi lakini ni bora kiongozi wa waislam wa eneo hilo pamoja na mwanachuoni mkuu wasimswalie kwa kutoa funzo kwa wengine kama hao.

• Swala ya maiti inaruhusiwa kuswaliwa msikitini, kama alivyofanya Mtume صلي الله عليه وآله وسلم imesimuliwa na Imam Muslim, lakini ilivyo sunna ni kuiswalia pembeni ya msikiti na ni vizuri kutenga eneo rasmi karibu na msikiti au karibu na makaburi kwa ajili tu ya kuswaliwa maiti ili msikiti usipate madhara ya kuchafuka n.k. Na ubora wa kupatikana eneo karibu na makaburi ni kwa ajili ya kuwarahisishia na kuwafanyia wepesi wazikaji Wallahu A’alam.

 

[Utangulizi] [Kumuosha maiti] [Kumkafini maiti] [Swala ya jenaza] [Kubeba jenaza na kuzika] [Kuomboleza na taazia]